I hope Don has a logo file? Project description Choose a text from the list Meet Litgloss participants Help
Main text Read some basic information For further reading
  "Hadithi" by David E. Diva
annotated by Musindu Kanya-Ngambi

WAVULANA WAWILI NA MACHUNGWA

Palikuwa na wavulana wawili, mmoja akiitwa Kasu na wa pili Ambari. Walikuwa wakikaa katika kijiji kimoja na kusoma katika skuli moja; walikuwa marafiki wakubwa sana.

Siku moja jioni, walikuwa wakitoka skuli na kurudi kijijini kwao. Walipokuwa wanapita katika shamba moja la michungwa, Kasu akamwambia Ambari, "Tazama machungwa hayo, yameiva vizuri sana. Je waonaje, hatuchumi machache tule, na mengine tuyachukue nyumbani?"

Ambari akamjibu, "La, michungwa hii si mali yetu wala ya jamaa zetu; kwa nini tuyachume? Huo ni wizi, haifai!"

Kasu akamwambia, "Ah lakini ipo njiani, na watu wengi hupita hapa; ni mali ya mtu ye yote."

Ambari akasema, "La, maana machungwa yenyewe yapo juu ya miti ya watu, hayapo njiani; huko ni mbali kabisa na kuokota kwa kawaida."

Walipokuwa wanajadiliana hivi, mtu mmoja akatokeza kichwa dirishani katika nyumba moja iyokuwapo karibu. Mtu yule aliitwa Hamisi, naye ndiye aliyekuwa mwenye shamba lile la michungwa, lakini wao hawa kumwona.

Ambari akasema, "Wakumbuka, Kasu, ya kuwa jana ulikuwa karibu na kupigana na Musa kwa sababu alichukua kalamu yako? Kwa nini, basi, wataka tuchukue machungwa ya watu?"

Kasu akasema, "Ah sijui, lakini mimi naona ya kuwa yapo kando ya njia. Kila mtu ana haki ya kuyachuma na kuyachukua."

Mara Hamisi, mwenye shamba, akacheka dirishani. Wavulana wale waliogopa sana. Kasu akakimbia, lakini Ambari alisimama pale pale alipokuwapo. Hamisi akachukua kikapu, akakijaza machungwa, akampa Ambari, akamwambia, "Chukua machungwa haya, na nusu yake kampe yule rafiki yako aliyekimbia. Nina hakika ya kuwa akiendelea na tabia yake mbaya ya kutokuwa na uaminifu atapotea; afadhali usishirikiane naye."

Ambari akamwambia Hamisi, "Asante sana, bwana, kwa machungwa haya na pia kwa maonyo yako."

Basi Ambari akayachukua machungwa yale, akampa Kasu, rafiki yake, nusu. Kasu alisikitikam sana kwa nia mbovu aliyokuwa nayo, na tangu siku ile akabadili mwenendo wake na kuwa mtoto mwema katika kila jambo.