|
"Oa," by Kaluta Amri Abedi
annotated by Musindu Kanya-Ngambi
Oa sioe anzali
mwenye mwenendo mbovu
Oa sioe jamali
wa akili tepetevu
Oa sioe jahili
jitu lenye ushupavu
Oa muovu sioe
oa mwana kwetu oa!
Oa akupendezaye
kwa umbile na tabia
Oa binti ya babaye
mtambuzi wa sheria
Oa mwali ajuaye
vyuoni aloingia
Oa muovu sioe
oa mwana kwetu oa!
Oa mke kufu yako
mnayefanana hali
Oa wa kikozi chako
wa asili na fasili
Oa binti ami yako
ikuwiyapo sahali
Oa muovu sioe
oa mwana kwetu oa!
Oa mrembo wa shani
mwenye hadhi na murua
Oa mwema na watani
uwezapo mgundua
Oa sioe muhuni
moto umejipalia
Oa muovu sioe
oa mwana kwetu oa!
Oa mtendee wema
Mkeo uliye naye
Oa uwe wa huruma
Roho yake ituliye
Oa mjaze heshima
Japo akuzuzukiye
Oa muovu sio
Oa mwana kwetu oa!
Oa wa macho laini
Yaengayo majimaji
Oa kwenda yu
Amin moyo akakufariji
Oa khasa mwana ndani
Asojua upitaji
Oa muovu sioe
Oa mwana kwetu oa!
Oa nakwiambia oa
Jaribu tena na tena
Oa kwa kuangalia
Na kumuomba Rabana
Oa upate tulia
Na kuepuka fitina
Oa muovu sioe
Oa mwana kwetu oa!
|